Mapigano yanaendela mashariki Congo DR
Mapigano mengine yamezuka karibu na mji wa Goma huko Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo-DRC, baada ya serikali ya DRC kupuuza madai ya
mazungumzo ya amani kutoka kundi la waasi wa M23.
Mwandishi wa habari wa Sauti ya Amerika-VOA anasema kulikuwa na
ufyatuaji risasi mkali Jumatatu kiasi cha kilomita tatu kutoka mji
wa Goma na karibu na uwanja wa ndege. Msemaji wa kundi la M23,Vianney
Kazarama aliiambia VOA kwamba kundi la waasi linadhibiti sehemu ya
kaskazini-mashariki mwa Goma.
Pia kuna ripoti za ufyatuaji risasi kwenye mpaka wa DRC na Rwanda.
DRC inaishutumu Rwanda kwa kuwasaidia waasi wa M23 huku Rwanda
ikiendelea kukanusha shutuma hizo.
Wapiganaji wa M23 wamesonga mbele kilomita chache kuingia Goma katika
muda wa siku chache zilizopita baada ya kuyarudisha nyuma majeshi ya
serikali na walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Wakati huo huo, Idara
ya Watoto ya Umoja wa Mataifa-UNICEF inasema vita vikali vinavyoendelea
huko Goma mashariki mwa DRC vimelazimisha maelfu ya watu ambao tayari
wamepoteza makazi yao kukimbia kwa mara nyingine.
UNICEF inasema ina wasiwasi juu ya athari za kisaikolojia ambazo
watoto wa Congo watakabiliwa nazo. Nona Zicherman mkuu wa UNICEF
anayeshughulikia masuala ya dharura huko Kinshasa anasema wasiwasi
wao mkuu ni hali ya wanawake na watoto ndani na karibu ya Goma, ambao
wameathirika na mapigano na pia wasiwasi juu ya usalama wa wafanyakazi
wao.
Anasema maelfu ya watu tayari wamekimbia maeneo ya watu waliopoteza
makazi yao kilomita kadhaa kutoka Goma.Zichermann anasema UNICEF inajua
kuwa kulikuwa na idadi kubwa ya raia waliokwenda Goma kutafuta hifadhi
na kwamba walikuwa wakiwasaidia katika kambi ya Kanyaruchinya iliyopo
nje ya Goma ambayo ni makazi ya takriban watu elfu 60.
Anasema japo hawana idadi kamili wanajua kuwa idadi kubwa ya raia wa
Kanyaruchinya na vijiji jirani pia wamekimbilia Goma na wamefika katika
sehemu kadhaa na wanaishi na familia zilizowapa hifadhi katika mitaa ya
Goma.
Category: news
0 comments