Hutakosa mambo haya kwenye filamu za Bongo
KWA Nigeria ambako ndiko kumeendelea zaidi kwa sasa katika suala la
filamu barani Afrika, walianza na filamu zilizojikita katika uchawi na
nguvu ya dini dhidi ya imani hizo za giza.
Baadaye wakaingia katika jamii, wakizungumzia uhusiano na usaliti katika ndoa na mambo mengine.
Hiyo kwao ilikuwa ni alama au utambulisho mkubwa vikiwa na lafudhi ya
kikwao katika kuzungumza Kiingereza. Kupitia filamu zao huwezi
kushindwa kubaini kuwa hawa ni waigizaji kutoka Nigeria.
Kwa upande wa filamu za Bongo, kuna mambo kadhaa ambayo ukiyaona
lazima ujue kwamba hiyo ni filamu ya Kibongo. Huwezi kuyakuta mambo hayo
kwa waigizaji wa sehemu nyingine.
Shuka nayo.
1. Jini likifika barabarani kabla ya kuvuka linaangalia pande zote
kushoto na kulia kisha linavuka barabara. Sijui kama ni sahihi.
Maana inasemekana kuwa jini ni kiumbe chenye miujiza na uwezo mkubwa
katika kutenda mambo yake hata kama kiumbe hicho kitajibadilisha kuwa
katika umbo la binadamu, lakini uwezo wake unabaki pale pale.
Sasa huyo jini anayeogopa magari katika kuvuka barabara ni jini gani?
2. Matajiri wetu katika filamu majumba yao yana askari badala ya
mageti yanayotumia umeme. Lakini jambo linaloshangaza zaidi ni walinzi
hao, mara nyingi hutambulishwa kwa utaahira au wachekeshaji huku
wakivalishwa uhusika wa kupenda masihara yanayokera. Mlinzi anakuwaje
mwendawazimu?
3. Utangulizi (Trailer) wa filamu inachukua hadi dakika 40.
4. Baada ya kutuunganishia Sehemu ya 1 na 2 ambazo ndio zimepewa jina
la Part 1 na Part 2, ukiangalia filamu ya Part 2 mwanzo tu unajua Part 1
ilikuwaje.
Hapa watazamaji wanahisi kuibiwa, maana yake ni kama daladala
linalotoka Kariakoo kwenda Kimara, halafu baada ya kufika Magomeni
abiria wanaambiwa litaishia Manzese ili kutoka hapo alipe tena nauli
mpya kwenda Kimara. Jamani safari moja nauli mara mbili?
5. Mademu wanaonekana wakiamka asubuhi wakiwa wamepambwa kabisa
(make-ups) usoni na hereni. Hii inaonyesha kuwa katika filamu zetu
hakuna kulala wala kugonga msosi. Haya nayo ni maajabu.
6. Waigizaji wa Bongo wakifika hotelini imezoeleka kuona wakiagiza
juisi au mvinyo isiyofunguliwa. Nadhani bajeti ya utengenezaji filamu ni
ndogo jambo linalofanya maigizo yazidi katika filamu zetu na watazamaji
kugundua ubovu.
7. Nusu saa mwigizaji anatembea, anafanya mazoezi, anakimbizwa mara ananunua vitu.
8. Wimbo wa malavidavi unaimba mpaka unaisha, hili ni katika filamu za Bongo Movie lakini filamu za wenzetu ni nadra kutokea.
9. Msanii yupo kijijini, maisha ni magumu lakini kichwani nywele
zimepakwa dawa na zinameremeta kwa mafuta. Kweli inaonyesha jinsi gani
wasanii hao wanavyojipenda, lakini kwa mtu anayewakilisha maisha magumu
ya kijijini anapaswa kuwa hivyo?
10.Wote wanaouawa kwa bunduki hupigwa kifuani au tumboni. Huwezi kuona sehemu nyingine. Au bunduki za Bongo zinachagua?
11.Jambazi lazima awe anavaa miwani nyeusi, koti jeusi na mvuta
sigara. Hivi kumbe wahalifu wote wa Bongo au duniani wana tabia
zinazolandana?
Hayo ndiyo matukio yanayojiri katika filamu za Bongo ambayo yanafanya mashabiki wajiulize kama kweli tupo makini na biashara au tunalipua.
Category:
0 comments