UEFA Champions League kurejea uwanjani wiki hii

damas venance | Tuesday, November 06, 2012 | 0 comments


Ligi ya mabingwa barani Ulaya ,Champions League ,Barca, Manchester United na Porto huenda zikakata tikiti zao kuingia katika michuano ya awamu ya mtoano wiki hii
Bayern Munich yazidi kupaa bila mpinzani ligi ya Ujerumani Bundesliga, mabingwa watetezi Borussia Dortmund bado yasua sua.na huko nchini Kenya timu tatu zawania ubingwa wa ligi ya nchi hiyo ikiwa umesalia mchezo mmoja tu hapo Jumamosi(10.11.2012)
Bayern Munich imeonesha msimu huu kuwa haina mpinzani, baada ya kupata ushindi wake wa tisa mwishoni mwa Juma baada ya kuizaba Hamburg SV kwa mabao 3-0. Baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Bayer Leversen wiki iliyopita, Bayern imejitutumua na kuongeza kasi katika msimamo wa ligi ambapo inaongoza sasa kwa points saba ikiiacha nyuma timu inayoifuatia Schalke 04 , ambayo ina points 20.
Einchracht Frankfurk inafuatia ikiwa nayo na points 20 na Bayer Leverkusen imeipiku Borussia Dortmund katika nafasi ya nne ikiwa na points 18 wakati mabingwa hao watetezi Borussia wako katika nafasi ya tano sasa wakiwa na points 16.
Michezo ya Jumapili (05.11.2012) ya kufunga mchezo huo wa 10 wa Bundesliga ilizikutanisha timu za Werder Bremen na Mainz 05 , na Bayer Leverkusen ilikuwa ikionyeshana kazi na Fortuna Dusseldorf. Werder Bremen ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mainz 05 na Leverkusen ikatwaa points zote tatu dhidi ya Fortuna Dusselsdorf kwa ushindi wa mabao 3-2.
Barcelona, Manchester United , FC Porto na pengine Malaga huenda wakakata tikiti zao kuelekea awamu ya mtoano katika Champions league wiki hii ikiwa timu hizo zitashinda michezo yake. Timu hizo nne zimekwisha shinda michezo yao yote mitatu ya mwanzo katika makundi yao na iwapao timu hizo zitashinda mchezo wa nne zitakuwa tayari zimekata tikiti zao tayari kwa michuano ya mtoano.
Schalke 04 , Borussia Dortmund na Shakhtar Donetsk huenda nazo zikajiweka katika mazingira mazuri ya kuingia katika michuano ya mtoano ikiwa zitapata ushindi , wakati mabingwa watetezi Chelsea , Manchester City na mabingwa wa zamani Juventus Turin ziko katika hali ngumu kidogo.
Champions League inafikia katika wakati muhimu sana na hatuwezi kuruhusu makosa mengine yoyote, amesema kocha wa Arsenal London , Arsene Wenger.Baada ya ushindi dhidi ya Montpellier na Olympiakos Piraeus katika michezo yao miwili ya awali katika kundi B, Arsenal iliteleza na kuangukia miguuni pa Schalke kwa kufungwa mabao 2-0 nyumbani wiki mbili zilizopita na ikishindwa tena katika ardhi ya Ujerumani matumaini ya timu hiyo yatakuwa yamewekwa katika mizani.
Chelsea ambayo ilikuwa na mwanzo wa kawaida wa utetezi wa taji lao kwa ushindi, sare na kufungwa, hawawezi tena kuhimili kipigo kingine nyumbani kwa Shakhtar Donetsk, baada ya kupata kipigo nchini Ukraine wiki mbili zilizopita.
Real Madrid inatafuta kulipiza kisasi kwa haraka dhidi ya Borussia Dortmund hapo kesho baada ya kupata kipigo bila kutarajia cha mabao 2-1 wiki mbili zilizopita nchini Ujerumani.
Ushindi wa Borussia Dortmund una maana kuwa timu hiyo inaongoza kundi la D ikiwa na points 7, moja zaidi ya Real , Ajax ikiwa na points 3 na Manchester City wakiwa na piint moja tu.
Utajiri wa Manchester City hautakuwa na maana iwapo timu hiyo itashindwa kutamba mbele ya Ajax Amsterdam kesho Jumanne katika uwanja wa Etihad.
Wakati huo huo wataalamu wa utabibu wanatengeneza kifaa cha kulinda uso ambacho kitamruhusu nahodha wa Borussia Sebastian Kiel kucheza katika mchezo kati ya timu yake na Real Madrid. Kiel alivunjika pua katika mchezo wa Bundesliga ambapo Borussia ilitoka sare ya bila kufungana na VFB Stuttgart, siku ya Jumamosi.
Kikosi cha Jose Mourinho kilijipasha moto kwa mchezo wa kesho kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Real Zaragoza katika La Liga nchini Uhispania lakini hawakuwa katika hali yao nzuri licha ya kiwango hicho cha mabao.ukosekana kwa Xabi Alonzo na Sami Khedira ambaye ni majeruhi , Mourinho aliteremsha uwanjani kikosi chenye baadhi ya wachezaji waliosajiliwa msimu huu kama Michael Essien na Luka Modric katika sehemu ya kati lakini hawakuwa na udhibiti unaohitajika.
Hata hivyo Alonzo atarejea kundini dhidi ya Borussia , lakini Khedira ana shaka kuanza mchezo huo.
Wakati huo huo mlinzi wa kati wa Barcelona Gerard Pique amerejea kundini baada ya kuwa majeruhi na sasa yuko fit kukabiliana na Celtic katika mchezo wa kundi G katika champions League.
Mabingwa watetezi Borussia Dortmund walitoka sare bila kufungana na VFB Stuttgart siku ya Jumamosi na kwa mabingwa hao sare ni sawa na kushindwa.

Category:

About GalleryBloggerTemplates.com:
GalleryBloggerTemplates.com is Free Blogger Templates Gallery. We provide Blogger templates for free. You can find about tutorials, blogger hacks, SEO optimization, tips and tricks here!

0 comments