Mkono adaiwa kumponza Makongoro Nyerere

damas venance | Tuesday, November 06, 2012 | 0 comments


Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikielekea katika Uchaguzi Mkuu wake Novemba 10, mwaka huu, makovu yanayotokana na chaguzi zilizofanyika yanazidi kujitokeza.
Tayari siri za kuwasilishwa kwa rufaa za kupinga matokeo katika ngazi tofauti zinafichuka, miongoni mwa hizo zikimhusu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary Nagu.
Nagu alishinda ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM kupitia wilaya ya Hanang’ `akimbwaga’ aliyekuwa mshindani wake wa karibu, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Mpaka sasa bado haijajulikana idadi ya malalamiko yaliyowasilishwa Makao Makuu ya CCM kuhusu kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi na matumizi ya rushwa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnaye, aliimbia k2b Jumapili jana kuwa, takwimu na taarifa hizo zinapaswa kutolewa na Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama.
Hata hivyo, Mkama alipopigiwa simu jana, alikataa kuzungumza kwa madai alikuwa msibani. “Nipo msibani tafadhali,” alisema kwa ufupi na kukata simu.
Lakini taarifa za ndani ya CCM zinaeleza kuwepo ‘vigogo’ na wanachama wa kawaida, walioshindwa katika nafasi tofauti za uongozi, kuwasilisha malalamiko yao, wakitaka matokeo yatenguliwe.
Miongoni mwa wanaotajwa ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere. Makongoro ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, alishiriki uchaguzi huo na kupata kura 422 dhidi ya Christopher Sanya, `aliyenyakua’ kura 481 na kutangazwa kushika wadhifa huo.
Hata Makongoro amekana kutoa malalamiko yake na kusema aliridhika na matokeo hayo.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kushindwa kwa Makongoro, kulitokana na kuungwa kwake mkono na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, viongozi kadhaa wa CCM mkoani Mara hususan wilayani Butiama, hawamuungi mkono, hivyo kupiga kura za hasira dhidi ya wafuasi wake, akiwemo Makongoro.
Ingawa Mkono hakupatikana kuelezea suala hilo, lakini Makongoro alithibitisha kuwa na maelewano mazuri na Mkono, na kwamba Mbunge huyo alitoa Shilingi milioni 31 kufanikisha uchaguzi mkoani Mara.
Makongoro alisema fedha hizo hazikumlenga yeye binafsi, bali chama kwa ujumla wake ili zifanikishe kugharamia mahitaji kama posho na vifaa.
Makongoro alisema wana-CCM wa mkoani Mara wanamheshimu Mkono, na hakuna sababu ya kumhusisha katika kushindwa kwake.
Badala yake alisema kushindwa kwake, kulitokana na nguvu kubwa ya utoaji rushwa kutoka kwa wapinzani kisiasa.
"Kwa ujumla watu wa Musoma tulio wengi tunamheshimu sana Mkono, hata kwenye uchaguzi alisaidia mamilioni ya fedha,” alisema.
Aliongeza, “wanaosema hawamheshimu huo ni uongo na hata kutochaguliwa kwangu hakutokani na mimi kuwa karibu naye."
Mbali na Makongoro ambaye pia ni Mbunge wa Afrika Mashariki, inaelezwa kuwa wagombea mbalimbali walioegemea upande wa Mkono walishindwa, huku washindani wake wakijigamba kuwa zamu ya Mbunge hiyo itakuwa mwaka 2015.
WENYEVITI WAMLALAMIKIA NAGU
Wilayani Hanang’ inaelezwa kuwa wajumbe 11 wa mkutano mkuu wa wilaya, wameelezea kutomuunga mkono Nagu, hivyo kutaka matokeo yaliyompa ushindi yatenguliwe.
Jitihada za Paparazzi wetu Jumapili kuwasiliana na Nagu ikiwemo kupitia simu yake ya mkononi,hazikufanikiwa kutokana na kuita mara kadhaa bila kupokewa.
Barua ya kupinga ushindi huo, iliandikwa Oktoba 19, mwaka huu, ikiwa ni tofauti na iliyotumwa Sumaye, ikiwa na kichwa kinachosomeka ‘kupinga matokeo ya uchaguzi nafasi ya mjumbe wa H/Kuu Taifa (Nec) wilaya ya Hanang’.
Wametaja sababu za kupinga matokeo hayo kuwa ni mazingira yenye kuashiria rushwa katika hatua ya kuchukua na kurudisha fomu, kampeni na uchaguzi.
Wajumbe wanaoonekana kusaini barua hiyo ni Martini Qossi Bayo, Odilo John, Eliuteri Claudi, Faustini Sule, Bakari Hamis na Gicharo Ng’wani.
Wengine ni Elisante Lorison, Tausi Idi, Kurdula Baasa, Frank Philipo na Phabiane John, kisha nakala yake ikatumwa kwa Makatibu wa CCM mkoani wa Manyara na wilayani Hanang’.
Walisema katika barua hiyo kuwa, siku ya uchukuaji fomu, mshindi aliwakusanya wajumbe kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya mabasi Katesh na kuwakabidhi baadhi yao trekta.
Inaelezwa kuwa mshindi alisema bila yeye kuwa mjumbe wa Nec, misaada kama hiyo haitaweza kupatikana wilayani humo.
“Kwa kupitia kauli zake hizo ambazo aliendelea kuzisema kwenye vikao vya kampeni, zilionyesha kuwa nia yake ni kuwahofisha wajumbe…” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Pia katika mazingira ya rushwa, Nagu anadaiwa kutoa mabati kwenye matawi ya Qabata (100), Qareda (100), Gawidu (200) na Endasiwald alipotoa Shilingi 1,000,000.
Wajumbe hao wanasema katika barua hiyo kuwa, mshindi alitumia ofisi ya umma na nyumbani kwake kufanya kampeni.
Malalamiko mengine ni kutumia nyadhifa zake kuwaita makatibu wa CCM wa kata na kufanya nao vikao vya mara kwa mara.
Shutuma nyingine zinazotajwa kwenye barua hiyo ni kusafirishwa kwa baadhi ya wajumbe wa mkutano wa uchaguzi baada ya CCM wilaya kujitoa katika jukumu hilo.
Hivi karibununi, Nape alikaririwa na vyombo vya habari akisema CCM inasubiri mchakato wa uchaguzi ukamilike, ndipo hatua ya kushughulikia mambo mbalimbali yakiwemo malalamiko hayo zifanyike.
Hata hivyo, kumekuwepo shinikizo na hitaji la baadhi ya wana-CCM kutaka matokeo yaliyolalamikiwa kufutwa, ili ufanyike uchaguzi wa marudio.
Lakini pia lipo kundi linalopendekeza kufutwa kwa matokeo yote, kwa madai kuwa sehemu kubwa ya uchaguzi huo iliathiriwa na vitendo vya rushwa.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugora, alisema matumizi ya fedha na rushwa yatakiwezesha chama hicho kupata viongozi wasiokuwa waadilifu, hivyo kuwa katika hatari ya ‘kutumbukia shimoni’ katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
KASHFA ZA RUSHWA
CCM inakabiliwa na kashfa za rushwa katika chaguzi zake kwa baadhi ya wanachama kutuhumiwa kukutwa wakihonga wajumbe.
Chaguzi hizo ndani ya chama hicho zilitawaliwa na kashfa ya tuhuma za rushwa na wanachama kufikia hatua ya kushambuliana kwa kushikana na kurushiana matusi na vijembe.
Chaguzi za jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT), Jumuiya ya Wazazi na Umoja wa Vijana (UV-CCM) ni kati ya zilizogubikwa na kashfa hizo.
Kwa jumuiya ya wazazi, wagombea walioshindwa waligoma kusaini fomu za matokeo kuonyesha kutokubaliana nayo na kuondoka bila kupanda jukwaani kutoa neno la shukurani.
Wagombea waliokuwa wakiwania nafasi hiyo ni Abdallah Bulembo, John Barongo na Martha Mlata. Aliyeshinda kinyang’anyiro hicho ni Bulembo.
Licha ya kashfa ya rushwa, baadhi ya wagombea wanadaiwa kutumia gharama kubwa kuwafadhili wapambe wao.
Makamu wa Rais, Dk. Ghalib Bilal, aliwaonya wajumbe kutokubali kununuliwa kwa rushwa hatua aliyosema inasababisha chama hicho kuingia kwenye fedheha.
WAPAMBE NA VIJEMBE
Vijembe na mipasho vilitawala nje ya ukumbi wa chuo cha Mipango, wapambe walitambiana kwa nyimbo zenye `vijembe’ kwa wagombea walio onekana kutoa upinzani mkubwa.
“Hatutaki watu waliostaafu wameshachoka kuja kutuongoza, hapa sio mahali pa kuja kupatia pensheni ya uzeeni,” alisikika mpambe mmoja akitamba.
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini anasema ingekuwa watu wanachukia rushwa, CCM isingefikia mahali ilipo sasa kwa kupoteza imani yake kwa umma.
JK AFEDHEHESHWA
Akifunga mkutano wa Jumuiya ya Wazazi mjini hapa, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alikemea tabia ya vitendo vya rushwa, mipasho na vijembe viiliyojitokeza kwenye chaguzi hizo.
Alisema tabia hiyo inaonyesha baadhi ya wanachama kutokuwa wakomavu na uvumilivu kisiasa.
Alisema lugha za matusi na kejeli kutumika katika kampeni zinaleta uhasama kwenye chama.
“Mbaya zaidi rushwa inapotumika katika uchaguzi, anayeona shilingi 30,000 , shilingi 70,000 inafaa inamnufaisha yeye mwenyewe na sio chama,”alisema Rais Kikwete na kuongeza sura ya chama chao inaadhirika sana.

Category:

About GalleryBloggerTemplates.com:
GalleryBloggerTemplates.com is Free Blogger Templates Gallery. We provide Blogger templates for free. You can find about tutorials, blogger hacks, SEO optimization, tips and tricks here!

0 comments