John Terry astaafu
John Terry, nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya soka ya England,
siku ya Jumapili alitangaza kustaafu kama mchezaji wa kimataifa.
Terry, ambaye ni mlinzi wa klabu ya Chelsea, na mwenye umri wa miaka
31, alitangazwa na mahakama ya Westminster mjini London mwezi Julai
kwamba hana hatia ya kutumia matamshi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Anton
Ferdinand, tukio ambalo lilifanyika katika mechi ya ligi kuu ya
Premier.
Lakini Terry, ambaye alishiriki katika mechi 78 za kimataifa, bado
huenda akaadhibiwa na chama cha soka cha FA, kutokana na utovu wa
nidhamu, huku chama kikiendelea kusikiliza kesi dhidi yake siku ya
Jumatatu.
Alisema: “Kuendelea kufuatia mashtaka dhidi yangu wakati mahakama
tayari imeshafanya uamuzi na kupata sina hatia….hayo hayanipi nafasi
kutimiza wajibu wangu.”
Mwezi Julai mahakama iliamua kwamba Terry hana hatia, lakini wiki
mbili baada ya hapo, chama cha FA kilimuandama kwa madai kwamaba
alitumia matusi, au maneno yasiyofaa, dhidi ya mlinzi wa QPR, mwezi
Oktoba, katika mechi iliyochezwa uwanja uliopo barabara ya Loftus.
Mahakama ilikuwa imesikiliza kesi dhidi ya Terry kuhusiana na madai
ya matamshi ya ubaguzi wa rangi, akimuelezea kama “mweusi” na maneno
mengine yasiyofaa.
Upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kikamilifu na pasipo na shaka yoyote kwamba Terry alitumia maneno hayo.
Lakini chama cha FA huenda kikamuadhibu kwa kuangalia tu kwamba
kulikuwa na uwezekano huo, na hasa ikiwa alimuelezea mchezaji mwenzake
kwa njia ambayo iligusia maneno kuhusu asili, au rangi yake.
Terry alimpigia simu meneja wa England, Roy Hodgson, kabla ya kuwasilisha wazi taarifa yake Jumapili jioni.
Terry alimrithi David Beckham kama nahodha mwaka 2006, lakini
alivuliwa wadhifa huo mwaka 2010, kufuatia madai kwamba alikuwa na
uhusiano wa kimapenzi na mke wa zamani wa mchezaji mwenzake katika timu
ya England, Wayne Bridge.
Category:
0 comments